Genesis 46

Yakobo Aenda Misri

1Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaka baba yake.

2Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”

Akajibu, “Mimi hapa.”

3Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yusufu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”

5Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha. 6Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. 7Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.

8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri:

Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.

9 Wana wa Reubeni ni:
Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.

10 Wana wa Simeoni ni:
Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.

11 Wana wa Lawi ni:
Gershoni, Kohathi na Merari.

12 Wana wa Yuda ni:
Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani).
Wana wa Peresi ni:
Hesroni na Hamuli.

13 Wana wa Isakari ni:
Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.

14 Wana wa Zabuloni ni:
Seredi, Eloni na Yaleeli.

15Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.


16 Wana wa Gadi ni:
Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.

17 Wana wa Asheri ni:
Imna, Ishva, Ishvi na Beria.
Dada yao alikuwa Sera.
Wana wa Beria ni:
Heberi na Malkieli.

18Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.


19 Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:
Yusufu na Benyamini.
20Huko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni,
Yaani Heliopoli (Mji wa Jua).
alimzalia Yusufu wana wawili, Manase na Efraimu.

21 Wana wa Benyamini ni:
Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.

22Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.


23 Mwana wa Dani ni:
Hushimu.

24 Wana wa Naftali ni:
Yaseeli, Guni, Yeseri na Shilemu.

25Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.

26Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita. 27Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yusufu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.

28Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yusufu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, 29gari kubwa zuri la Yusufu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yusufu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.

30Israeli akamwambia Yusufu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”

31Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. 32Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ng’ombe pamoja na kila kitu walicho nacho.’ 33Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ 34Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”
Copyright information for SwhKC